Na: Judith Damas
Wajumbe wa kamati ya kudhibiti UKIMWI ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, leo tarehe 16 Februari 2022, wamefanya ziara ya kukagua vituo vinavyojishughulisha na utekelezaji wa kudhibiti UKIMWI vilivyopo Kata ya Buguruni Jijini Dar es Salaam .
Kamati hiyo inayoongozwa na Naibu Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Mhe.Saady Khimji iliweza kutembelea vituo viwili vinavyojishughulisha katika kuimarisha Shughuli za kuthibiti UKIMWI ambovyo ni Kituo cha afya Buguruni ambacho kina kitengo cha huduma rafiki kwa vijana na Kamati ya kudhibiti UKIMWI Kata ambapo katika kituo cha afya Buguruni wameweza kupambana kudhibiti UKIMWI kwani wameweza kuanzisha huduma rafiki kwa vijana na pia wameweza kuanzisha kikundi cha Buguruni Youth Peer Educators (BUYOPE) ambacho hutumia sanaa mbalimbali kama ngoma pamoja na maigizo lengo likiwa ni kutoa elimu kwa vijana wengine juu Kujitambua na kujikinga dhidi ya UKIMWI, ukatili wa kijinsia, elimu juu ya matumizi ya dawa za kulevya, elimu juu ya kutumia uzazi wa mpango pamoja na kujikinga dhidi ya magonjwa ya mlipuko ikiwemo ugonjwa wa Korona (COVID-19).
Akizungumza katika ziara hiyo Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye ni Naibu Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam Mhe. Saady Khimji ameweza kumpongeza Mganga Mfawidhi wa Kituo cha afya Buguruni pamoja na timu nzima ya madaktari na wauguzi kwa kuweza kuanzisha huduma rafiki kwa vijana kiafya na kijamii ambapo huduma hii itawaleta karibu vijana wetu hivyo kuongeza nguvu kazi ya Taifa letu.
Mhe. Khimji amesema "Nawapongeza sana vijana wa Buguruni Youth Peer Educators (BUYOPE) kwa shughuli mnazozifanya za kuelimisha Jamii juu ya kulinda afya zao pia kwa kazi nzuri mnayoifanya ya kuwaelimisha baadhi ya vijana wenye maambukizi ya UKIMWI lengo likiwa ni kuwasaidia, hivyo kwa vijana waliokwisha pata maambukizi ya virusi vya UKIMWI waweze kuunganishwa katika Konga ili kuweza kushirikiana na wengine katika kutekeleza shughuli za Konga."
Sambamba na hilo Mhe. Khimji ameeleza kua kwa kushirikiana na Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam watahakikisha wanashirikiana na vikundi hivi kwa kuwawezesha vijana hawa kupata mkopo na pia watahakikisha kamati zote za kudhibiti UKIMWI ngazi ya Kata zina fanya kazi kikamilifu lengo likiwa ni kuimarisha afya za wananchi hususani vijana ambao ni nguvu kazi ya Taifa na ambao ndio waathirika wakubwa wa majanga haya.
Naye Mratibu wa UKIMWI wa Halmashauri ya Jiji la DSM, Ndug. Barnabas Kisai ametoa shukrani zake kwa wajumbe wa Kamati ya UKIMWI ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaa na kuahidi ushirikiano katika kutekeleza yote aliyoagizwa kuyafanya ili kupunguza maambukizi ya usambaaji wa virusi vya UKIMWI na hatimaye kuongeza nguvu kazi ya Taifa.
Kwa upande wake Mratibu wa vijana Kituo cha afya Buguruni Sr. Janeth Nyera ameeleza kua huduma rafiki kwa vijana imeweza kuwa chachu kubwa kwa vijana kwani wameweza kuwaunganisha vijana wa makundi na rika mbalimbali wenye matatizo mbalimbali ya kiafya na kijamii ambao walikua na hofu ya kueleza matatizo yao kipindi cha nyuma hivyo kwa kushirikiana na vijana hao wameweza kuelimisha na kuwasaidia vijana wengi pia ameeleza kuwa vijana hao wameweza kutengewa siku yao maalumu ya kufika kituoni hapo ambayo ni siku ya Jumamosi hivyo ameahidi kushirikiana kikamilifu na Kamati ya kudhibiti UKIMWI ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na amemtaka mwakilishi wa Konga kuweza kuwatembelea kila Jumamosi ili kukutana na vijana walio na maambukizi ya VVU lengo likiwa ni kuwaunganisha na konga na kuwaelimisha zaidi ili wasikate tamaa ya maisha.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.