Kamati ya Lishe Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam leo Machi 15, 2024 imefanya Kikao cha kawaida cha Kujadili taarifa za utekelezaji wa kazi za Afya na lishe kwa kipindi cha Robo ya pili kuanzia Oktoba hadi Desemba 2023.
Akifungua kikao hicho kilichofanyika kwenye ukumbi wa Mikutano wa Arnatoglou kwa niaba ya Mkurugenzi, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam Tabu Shaibu amesema kuwa Halmashauri ya Jiji inatekeleza maagizo ya upatikanaji wa lishe kwa vitendo kwani Serikali ya Tanzania imedhamiria kuendelea kulipa umuhimu wa kipekee suala la lishe bora nchini ili kuhakikisha Tanzania inakuwa na uchumi imara kupitia maendeleo ya viwanda, hivyo elimu ya Lishe itasaidia uwepo wa watu (nguvu kazi) wenye afya njema ili kuwawezesha kufanya kazi kwa bidii na Kuchochea maendeleo ya nchi.
Katika kikao hicho Divisheni mbalimbali ziliwasiliisha taarifa za utekelezaji wa kazi za Afya na lishe kwa kipindi cha robo ya pili ambapo baada ya taarifa hizo Kamati iliweza kujadili na kutoa maelekezo kwa Divisheni ya Elimu Sekondari kuhamasisha zaidi suala la lishe kwa wanafunzi kwani inaonekana Shule nyingi za Sekondari wanafunzi hawapati mlo kamili.
Kwa upande wake Kaimu Mratibu wa Lishe wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam Neema Mwakasege ameeleza kuwa Kamati imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kutoa elimu ya lishe kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari, wazazi na walezi na kuahidi kuendelea kutoa Elimu hiyo ikiwa ni sehemu ya kutekeleza dhamira ya Jiji la DSM ya kuhakikisha elimu inatolewa katika maeneo yote na watu wa rika zote.
Katika hatua nyingine, wajumbe wa Kamati Kuu ya Lishe waliweza kuchangia maoni Yao juu ya upatikanaji wa chakula mashuleni kwa kuwataka wazazi na walezi kuwa kipaumbele katika kuchangia ili watoto wasiweze kula vyakula ambavyo sio vya shule.
Katika upande wa Idara ya Mifugo imesisitiza ulaji wa nyama salama ambayo imepimwa vizuri nakuthibitishwa kwaajili ya kula.
Aidha, katika kikao hicho wajumbe walikubaliana katika kuongeza jitihada zaidi katika kuandaa programu za kuhamasisha na kutoa elimu za mara kwa mara kwa wananchi juu ya masuala ya lishe hususani mashuleni na kwa mama lishe ili kuboresha Afya za wananchi kwa maendeleo ya Nchi pamoja na kufanya ziara kutembelea mashule pamoja na viwanda ili kujionea kwa ukaribu utekelezaji wa shughuli za lishe.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.