Kamati ya Mipango Miji na Mazingira ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, leo Oktoba 25, 2023 imefanya Ziara ya ukaguzi wa Mazingira na Upangaji Miji ikiwa ni sehemu ya majukumu ya Kamati kusimamamia matumizi bora ya ardhi kwa kuzingatia mpango wa matumizi ya ardhi (Master Plan) ya Jiji na kusimamia matumizi sahihi ya Miundombinu iliyopo pamoja na usafi wa mazingira, hii ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa miradi pamoja na utunzaji wa Mazingira kwa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa kipindi cha robo ya kwanza ya Mwaka wa Fedha 2023/2024 ulioanza Julai hadi Septemba 2023.
Wakiwa kwenye ziara hiyo, Kamati iliweza kutembelea kiwanda cha maji cha Dew Drop kilichopo Buguruni na Kiwanda cha Unga cha Azania kilichopo Tabata Matumbi lengo likiwa ni kukagua hali ya usafi wa Mazingira kwa ustawi na usalama wa wafanyakazi pamoja na Wananchi wanaozungukwa na viwanda hivyo.
Kwa upande mwingine, Kamati pia ilitembelea na kukagua eneo la uwekaji wa vigae (pavings) kwenye njia ya watembea kwa mguu Kata ya Kivukoni ambapo takribani shilingi milioni 600 fedha kutoka Mapato ya Ndani ya Halmashauri zimetumika kuteleza mradi huo unaoendelea katika Mitaa ya Luthuli, Sokoine na Ardhi.
Naye, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Nyansika Getama akifanya majumuisho ya ziara hiyo amesema, "Leo tumetembelea baadhi ya miradi inayosimamiwa na kutekelezwa na Halmashauri ya Jiji la DSM ambapo tumeweza kuridhishwa na utekelezaji huo japo kuna marekebisho madogomadogo yakukamilisha hususani katika suala zima la utunzaji wa mazingira kwa baadhi ya maeneo ya viwandani na baadhi ya maeneo yanayotiririsha maji machafu yafanyiwe utekelezaji."
Aidha Kamati imeagiza wataalamu wa Divisheni za Mipango Miji na Mazingira kuandaa taarifa sahihi endapo eneo la Halmashauri ya Jiji lililopo TRC Gerezani kama limevamiwa huku wakiitaka Divisheni ya Mipango Miji kuandaa utaratibu wa kupitia ramani ili kubainisha maeneo ya wazi na yaliyo vamiwa ya Halmashauri, pia kamati imeagiza wataalamu kutoka Divisheni ya Mazingira kuhakikisha viwanda vyote vinavyotiririsha maji taka vinapigwa faini kwa mujibu wa sheria na kanuni zinavyoelekeza.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.