Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ilala chini ya Mwenyekiti wake Ndg. Said Sidde leo tarehe 15 Agosti, 2024 imefanya ziara ukaguzi wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Jiji la DSM ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi.
Miradi iliyotembelewa na Kamati hiyo ni pamoja na Mradi wa Ujenzi wa ghorofa sita Shirika la Uchumi na Maendeleo la Jiji la DSM wenye thamani ya shilingi Bilioni 30, ujenzi wa Barabara ya Bima – Kimanga kiwango cha lami yenye urefu wa mita 400 wenye thamani ya milioni 593 ikiwa ni pamoja na ujenzi wa mitaro na kuweka taa za kisasa, Ujenzi wa vyumba vya madarasa 20 na matundu ya vyoo 45 katika Shule ya Sekondari Bonyokwa wenye thamani ya milioni 539.
Akiongea wakati wa ziara hiyo, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ilala Ndg. Said Sidde amesema “Naipongeza Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam wakiongozwa na Mstahiki Meya na Mkurugenzi, pia nampongeza Mkuu wa Wilaya ya Ilala kwa ongeze kubwa la mapato na kusimamia na kutekeleza miradi kwani thamani ya fedha inaonekana na miradi inatekelezwa kwa kiwango cha juu. Hii inaonyesha ni jinsi gani Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inavyotekelezwa kwa kasi hivyo niwaombe kukamilisha miradi ambayo bado inasuasua hasa barabara Bima - Kimanga kwani barabara hii ni muhimu kwa wakazi wa Tabata kwa usafirishaji.”
Pia, Ndg. Said Sidde ameongeza “Natoa maelekezo kwa viongozi na watendaji wa Halmshauri ya Jiji la DSM kuhakikisha mnachagua wakandarasi wazawa wenye uwezo na uzoefu ili waweze kukamilisha miradi kwa ubora na wakati ili wananchi waweze kufurahia huduma. Pia natoa wito kwa maeneo ya wazi yanayomilikiwa na Halmshauri mkaribishe wawekezaji wawekeze ili kuongeza ajira na mapato ya Halmashauri na Nchi kwa ujumla."
Awali akiwasilisha taarifa ya miradi na utekelezaji wa Ilani kwa Mwenyekiti wa CCM Wilaya pamoja na wajumbe wa Kamati ya Siasa Wilaya ya Ilala, Mkuu wa Wilaya ya hiyo Mhe. Edward Mpogolo ameeleza kuwa “Viongozi tuna deni kwa Rais wa Jamhuri Ya Muungano wa Tanzania, kwa sababu fedha zote zilishatolewa. Hivyo ni matumaini yake kuona miradi yote katika sekta za Elimu, Afya, na Barabara inakamilika kwa wakati. Hivyo nitoe wito kwa wasimamizi wa miradi kujituma na kufanya kazi kwa bidii ili kukamilisha miradi kwa manufaa ya wananchi wa Ilala na maeneo ya jirani.”
Kwa upande Mstahiki Meya Mhe. Omary Kumbilamoto amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa pesa anazotoa kwa Halmashauri yetu, pia amemshukuru Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ilala kwa ziara aliyoifanya huku akimuhakikishia kutekeleza maelekezo yote aliyoyatoa kwa manufaa ya wananchi.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.