Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Edward Mpogolo, amesema kuwa Ofisi yake , Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji, kwa kushirikiana na Benki za NMB na CRDB wako tayari kushuka hadi ngazi ya Kata na Mitaa kwa ajili ya kutoa elimu kuhusu mikopo ya asilimia 10 inayotokana na mapato ya ndani, ili kuhakikisha kila mwananchi anapata fursa kwa kufuata taratibu na miongozo ya utoaji wa mikopo hii kwa kupitia mfumo jumuishi.
Akizungumza leo tarehe 20 Juni 2025 katika hafla ya utoaji wa mikopo isiyo na riba kwa mfumo jumuishi, Mhe. Mpogolo amesema kuwa elimu hiyo itatolewa na timu ya viongozi wa Jiji ikijumuisha Ofisi yake, Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, pamoja na watendaji wa Halmashauri ya Jiji kwa kushirikiana na Benki hizo.,lengo ni kuwafikia wananchi moja kwa moja na kuwawezesha kufahamu kwa kina taratibu za kupata mikopo hiyo.
Elimu hiyo itajikita katika namna ya kujaza fomu za maombi, utaratibu wa uundaji wa vikundi, taratibu sahihi za urejeshaji wa mikopo hiyo, ikiwa ni pamoja na kupata elimu ya matumizi ya TEHAMA katika uombaji wa mikopo hiyo.
"Tutashuka chini kwa Wananchi yaani kata kwa kata, na mtaa kwa mtaa, kuhakikisha kila muhitaji au mnufaikaji anapata mkopo, ili aweze kuinuka kiuchumi. Hatutakubali hata mmoja akose nafasi hii kwa kukosa uelewa." amesema Mkuu huyo wa Wilaya
Mheshimiwa Mpogolo amesema pia juhudi hizo ni utekelezaji wa maelekezo ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ameendelea kusisitiza umuhimu wa mikopo hiyo kama nyenzo ya kuwawezesha wananchi kiuchumi na kupunguza umaskini kupitia vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.