Wakazi wa Jiji la Dar es Salaam wameungana na Wananchi wengine ulimwenguni kote katika kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani. Maadhimisho haya katika ngazi ya Mkoa yamefanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.
Siku ya Mazingira Duniani husheherekewa Ulimwenguni kote kila tarehe 5 Juni, kila mwaka. Madhumuni ya maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani ni kuhamasisha jamii duniani kote kuelewa masuala yahusuyo Mazingira na pia kuhamasisha watu wa jamii mbalimbali duniani kuwa mstari wa mbele katika kuchukua hatua za kuhifadhi na kulinda mazingira.
Awali, maadhimisho hayo yalitanguliwa na maandamano kutokea viwanja vya Posta ya zamani hadi viwanja vya Mnazi Mmoja na kupokelewa na mgeni rasmi Mhe. Sophia Mjema, Mkuu wa Wilaya ya Ilala ambaye alimuakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Paul C. Makonda.
Mhe. Sophia Mjema baada ya kupokea maandamano na utambulisho wa viongozi mbalimbali wa Serikali, wadau wa mazingira katika sekta binafsi na za umma alitoa shukrani za dhati kwa maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani na kupongeza juhudi za urejelezaji taka na kuwa mali zinazofanywa na wadau mbalimbali wa mazingira jijini Dar es Salaam.
Maadhimisho ya Siku ya Mazingira jijini Dar es Salaam yalianza tangu tarehe 31 Mei, 2017 na kufikia kilele tarehe 5 Juni, 2017 ambapo shughuli mbalimbali zinazohamasisha utunzaji wa mazingira katika maeneo mbalimbali zikiwemo:
Mgeni rasmi aliendelea kueleza kwamba shughuli hizo ziliambatana na ukaguzi wa vifaa vya makampuni ya usafi na uhamasishaji kwa wananchi katika masula ya uhifadhi na usafishaji wa mazingira yanayowazunguka.
Mhe. Mjema ametoa wito kwa Wananchi wa Jiji la Dar es Salaam kufahamu kwamba wao wana wajibu wa kuzuia madhara na mabadiliko hasi katika Mazingira na kuwaasa watendaji na viongozi wa Serikali waliopewa dhamana ya kusimamia sheria za kisekta na sheria ndogo za mazingira kuhamasisha jamii kufanya mazingira yao kuwa salama na masafi kwa lengo la ustawi wa maisha yetu na vizazi vyetu.
Akihitimisha hotuba yake, Mhe. Sophia Mjema amewaomba wananchi wote wa Jiji la Dar es Salaam kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano ili kuifanya nchi yetu kuwa nchi ya viwanda, kuongeza mapambano dhidi ya dawa za kulevya, kuhimiza usafi wa mazingira na kuondoa utoroshaji wa raslimali katika nchi yetu.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Bi. Sipora Liana pia alipata fursa ya kutembelea banda la vijana wajasiriamali wanaorejeleza taka ngumu na kuwa bidhaa mbalimbali na kuwaeleza mpango wa Halmashauri ya Jiji wa kujenga miundombinu ya viwanda vidogo vidogo ili kuweza kuwafikishia huduma muhimu vijana na wanawake kwa pamoja ili wajikwamue kiuchumi, kujiongeza kipato na kupunguza tatizo la ajira hasa kwa vijana na kina mama kwa kuwarasimisha wajasiriamali hawa wadogo ambao wengi hawako rasmi kwa kukosa sehemu za kufanyia kazi.
Kauli mbiu inayoongoza maadhimisho haya kimataifa ni “Connecting People to Nature”. Kwa Kiswahili ni: “Mahusiano Endelevu Kati ya Binadamu na Mazingira”. Kauli mbiu hii inahamasisha jamii kuwa na urafiki endelevu na mazingira asilia ambapo kila mtu anapaswa kutambua, kufurahi, kujivunia na kulinda uzuri wa mazingira asilia yetu na kuhamasishana kuyatunza na kuhifadhi.
Pamoja na kauli mbiu ya kimataifa, kauli mbiu ya maadhimisho ya Siku ya Mazingira mwaka huu kitaifa ni "Hifadhi ya Mazingira: Muhimili kwa Tanzania ya Viwanda.” Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani mwaka 2017 katika ngazi ya Taifa yanafanyika kijijini Butiama Mkoani Mara, ambako Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, alizaliwa, kukulia na kuzikwa.
Madhumuni ya kupeleka maadhimisho haya Butiama ni kumuenzi Baba wa Taifa kwa sababu alikuwa mwanamazingira namba moja nchini mwetu lakini pia tunaenzi na kukumbuka mchango wake mkubwa katika masuala ya kuhifadhi mazingira nchini. Bila msimamo wa Mwalimu Nyerere kuhusu hifadhi ya mazingira, bila falsafa yake kuhusu uhifadhi, na bila hatua madhubuti alizochukua kulinda mazingira ya asili ya nchi yetu mapema kabisa tulipopata uhuru, nchi yetu isingekuwa inasifika kwa uzuri wake na vivutio vyake.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.