Kuelekea kilele cha Maadhimisho ya sherehe za miaka 60 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yenye Kaulimbiu “Tumeshikamana na Tumeimarika kwa Maendeleo ya Taifa letu”, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imefanikiwa kupanda miti 200 katika Shule ya Msingi Magoza, Shule ya Sekondari Magoza na Kituo cha Polisi cha Tembomgwaza. Kazi hiyo pia imefanyika katika Zahanati ya Kinyerezi, Kata ya Kinyerezi ambapo miti 150 imepandwa katika eneo hilo.
Shughuli hizo za upandaji miti zimeongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mhe. Edward Mpogolo. Upandaji huo miti katika maadhimisho ya Miaka 60 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni muendelezo wa utekelezaji wa mpango wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam wa wa kupanda miti 1,500,000 kila mwaka.
Viongozi wengine walioshiriki katika shughuli za upandaji wa miti hiyo Pamoja na watumishi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, wananchi na wadau mbalimbali ni Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Omary Kumbilamoto na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Jomaary Satura.
Shughuli zingine zilizofanyika chini ya usimamizi wa Mhe. Mpogolo katika maadhimisho ya sherehe hizo ni kufanya usafi katika makutano ya Barabara za Nkurumah na Lumumba, Barabara ya Morogoro na eneo la Mnazi Mmoja. Wananchi na wadau katika sekta ya mazingira na udhibiti wa taka ngumu nao walijitokeza pia kushiriki katika kazi hii
Kwa upande wa michezo na burudani, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam iliandaa na kusimamia maonesho ya ngoma za asili yaliyohudhuriwa na wananchi wengi, mashindano ya uandishi wa insha kwa wanafunzi wa Shule za Msingi na Sekondari, maonesho ya vyakula vya asili na mashindano ya mpira wa miguu.
Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar uliundwa tarehe 26 Aprili 1964 na ulizinduliwa rasmi na Mwalimu Julius Kanbarage Nyerere, Rais wa Jamhuri ya Tanganyika na Sheikh Abeid Amani Karume, Rais wa Serikali ya Mapinduzi katika Ukumbi wa Mikutano wa Karimjee, Dar es Salaam. Hivyo kwa maadhimisho ya sherehe hizo kufanyika Dar es Salaam mwaka huu ni tukio jingine la kihistoria ambalo kamwe halitasahaulika
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.