Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Sipora Liana, amewataka watumishi wake kujituma katika kufanya kazi, kuongeza bidii, na kuwa wabunifu katika utoaji wa huduma bora kwa wananchi na wadau mbalimbali wa Halmashauri.
Ameyasema hayo leo tarehe 24 Juni, 2019 wakati akihitimisha Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yaliyoanza tarehe 16-23 Juni, 2019 katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam yenye kauli mbiu; "Uhusiano kati ya uwezeshaji wa vijana na usimamizi wa masuala ya uhamiaji: Kujenga utamaduni wa Utawala Bora, matumizi ya TEHAMA na ubunifu katika utoaji wa Huduma Jumuishi."
Aidha alieleza kuwa watumishi wote wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam wanatakiwa kutumia maadhimisho hayo kujikumbusha kuhusu haki na wajibu wao kisheria huku wakizingatia kanuni na taratibu mbalimbali za utumishi wa umma katika utoaji wa huduma bora.
Katika hatua nyingine Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji Dar es Salaam alitumia fursa hiyo ya kukutana na watumishi wake wote kuwaeleza maendeleo ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa ikiwemo ujenzi wa Kituo Kikuu cha Kimataifa cha Mabasi katika eneo la Mbezi Luis.
Miradi mingine aliyoieleza kwa watumishi hao ni ujenzi wa miundombinu katika eneo la kupumzikia DRIMP inayohusisha ukumbi wa nje wa maonyesho ya kiutamaduni, ukumbi wa ndani wa mikutano pamoja na ujenzi wa maduka 19 ya biashara na mradi wa ujenzi wa viwanda vidogo vidogo katika eneo la Mwananyamala ambao unahusisha ujenzi wa viwanda vidogo vidogo sita, choo cha umma matundu 10, mgahawa na maduka ya biashara saba.
Watumishi mbalimbali wa Halmashauri ya Jiji Dar es Salaam wametumia fursa hiyo kuwasilisha maoni yao na changamoto wanazozipata na waliweza kupatiwa majibu ya ufafanuzi ambayo kwa kiasi fulani yaliwaridhisha.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.