Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Jumanne Shauri, amemshukuru na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimwa Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kufungua milango zaidi inayowaruhusu watu mbalimbali kutoka Miji rafiki ya nje ya nchi kutembelea Tanzania. Shauri ameyasema hayo alipokuwa akiongea na waandishi wa Habari katika mkutano aliouitisha leo tarehe 20 Juni, 2022 kuwajulisha waandishi wa habari kuhusu ujio wa wageni zaidi ya 30 kutoka katika Jiji la Hamburg nchini Ujerumani watakaofanya ziara katika Jiji la Dar es Salaam tarehe 30 Juni, 2022 hadi tarehe 03 Julai, 2022.
Akiongea na waandishi hao wa Habari katika ukumbi wa mikutano wa Old Boma Jijini Dar es Salaam, Shauri amesema kwamba lengo ujio wa ujumbe huo ni kufanya maadhimisho ya miaka 12 ya uhusiano wa Miji Dada kati ya Jiji la Hamburg na Jiji la Dar es Salaam.
“Katika maadhimisho hayo, pande zote mbili zitasheherekea mafanikio yaliyofikiwa hadi sasa katika utekelezaji wa miradi ya mabadiliko ya tabia ya nchi, afya, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji , michezo na utamaduni, elimu, utalii, stadi za kazi za wanawake, vijana na watu wenye mahitaji maalumu” amesema Shauri.
Katika uhusiano huo Mkurugenzi huyo amesema kumekuwa na fursa nyingi kwa Jiji la Dar es Salaam kufanya ziara za kujifunza na kubadilishana uzoefu wa utendaji kazi katika Jiji la Hamburg na wenzao wa Hamburg pia kufanya ziara kama hizo katika Jiji la Dar es Salaam. Ziara hizo zimewashirikisha pia wadau kutoka asasi za kiraia na mashirika yasiyokuwa ya Serikali.
Aidha, maadhimisho ya Uhusiano wa Miji Dada kati ya Jiji la Dar es Salaam na Jiji la Hamburg, ulioanzishwa tarehe 01 Julai, 2010 baada ya Mamlaka za Majiji hayo kuridhia kuanzishwa kwa uhusiano huo, yanatarajiwa kufanyika tarehe 30 Juni, 2022 hadi tarehe 03 Julai, 2022 ambapo viongozi wa wa majiji hayo mawili watasaini makubaliano ya ya kudumisha uhusiano huo kwa kutoa nafasi kwa wadau wengine zaidi kunufaika na fursa zinazojitokeza kupitia uhusiano huo.
Akihitimisha mkutano huo, Shauri amesema “Sherehe za maadhimisho ya uhusiano huo zitafanyika siku ya Jumapili, tarehe 03 Julai, 2022 katika viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam, hivyo wananchi wote wanakaribishwa kushiriki na kutumia fursa hiyo kwa manufaa ya Jiji la Dar es Salaam.”
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.