Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa miaka minne mfululizo imepata hati safi kupitia ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG) katika ukaguzi wa taarifa za mapato na matumizi za Halmashauri ya Jiji.
Hayo yamebainika wakati wa mkutano wa Baraza maalum la Madiwani wa Halmasahauri ya Jiji la Dar es Salaam liloketi leo tarehe 05 Juni, 2020 katika ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kujadili taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2018/2019.
Naibu Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam Mheshimiwa Abdallah Mtinika amesema Halmashauri hiyo chini ya Mkurugenzi bi. Sipora Liana imeendelea kupata hati safi toka ofisi ya CAG.
“Kwa Miaka minne Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imepata hati safi ya hesabu zake kutoka kwa CAG, hatua hii ni heshima kubwa sana kwa mkoa wetu wa Dar es Salaam, alieleza Mtinika".
Aidha, Mtinika amesema hatua ya kupewa hati safi kwa Halmashauri ya Jiji ni kutokana na utekelezaji wa maagizo na miongozo ya Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli ya kuzitaka Halmashauri kusimamia mapato na matumizi ya fedha za Serikali.
Naye Meya wa Manispaa ya Ilala Mheshimiwa Omary Kumbilamoto ambaye ni mjumbe wa Baraza hilo amempongeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam bi. Sipora Liana kwa utendaji wake ambao umepelekea Halmashauri hiyo kupewa hati safi na ofisi ya CAG.
“Hii inatokana na ushirikiano ambao tunaupata kutoka kwa Mkurugenzi wa Jiji Waheshimiwa Madiwani pamoja watendaji wote wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, nawapongeza sana Jiji kwa kuibua mradi stendi ya kisasa ambao utaboresha taswira ya Dar es Salaam na mshukuru sana Rais Magufuli kwa kutoa fedha nyingi kwa mradi ule” amesema Kumbilamoto.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.