Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Edward Mpogolo amewataka Watendaji wa Kata kuhakikisha wanasimamia na kuhamasisha utekelezaji wa afua za lishe katika Wilaya hiyo ili kutokomeza udumavu na utapiamlo kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano.
Mhe. Mpogolo ametoa wito huo leo Juni 20, 2024 wakati wa kikao cha kawaida cha Tathmini ya Mkataba wa lishe kilichofanyika ukumbi wa Arnatoglou Jijini Dar es Salaam lengo likiwa ni kupitia viashiria vyote vilivyopo katika Mkataba wa lishe vilivyotekelezwa kwa robo ya tatu ya Mwaka wa Fedha 2023/2024 (Januari-Machi 2024).
Akizungumza wakati wa kikao hicho, Mhe. Mpogolo amewataka wajumbe wa kikao hicho kufahamu kuwa lishe ndiyo msingi wa kila kitu katika jamii na kwamba kikao hicho ni muhimu sana katika uboreshaji wa lishe katika Jamii ili kuondokana na udumavu na utapiamlo kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano. “Napenda kuipongeza Idara ya Afya pamoja na watendaji wote kwa utekelezaji wa afua za lishe kwa kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu lishe bora. Hivyo niwatake Watendaji wa Kata kuendelea kufanya vikao na kutoa elimu kuhusu lishe kwenye Kata zenu na kuweka maazimio kuhusu utekelezaji wa afua za lishe ili kufikia malengo”.
Sambamba na hilo, Mhe. Mpogolo Ameeleza kuwa ukosekanaji wa chakula kwa wanafunzi ni miongoni mwa sababu za udumavu na kuwasihi Watendaji wa Kata kuwaelimisha wazazi wajue umuhimu wa chakula shuleni kwa watoto wao kwa kuhakikisha wanasimamia shule zote zinatoa chakula na wanafunzi wote wanapata chakula cha Mchana pindi wakiwa shuleni pamoja na kuhamasisha wazazi kutoa michango ya chakula kwa watoto wao sambamba na kufanya kampeni ya lishe bora kwa watoto huku akiwataka kufanya ziara mashuleni juu ya maadili, usalama, afya pamoja na masuala ya lishe kwa watoto ili waweze kuelewa masuala mbalimbali hususani masuala ya ukatili wa kijinsia ambayo yamekua yakiwakabili watoto wangi.
Awali akisoma taarifa ya tathmini ya utekelezaji wa mkataba wa lishe kwa ngazi ya Wilaya, Mratibu wa Lishe Jiji la Dar es Salaam Bi. Flora Mgimba ameeleza kuwa viashiria vyote 11 vinavyopimwa katika utoaji wa huduma za lishe vimetekelezwa vizuri kwa kufikia hali nzuri ya utekelezaji kwani mafanikio yaliyopatikana kwenye utekelezaji kwa ngazi ya Kata ni kuimarika kwa ushirikiano kwa ngazi ya vituo, jamii na viongozi wa ngazi mbalimbali toka Wilaya hadi Mitaa pamoja na lishe kuwa suala mtambuka na kuongelewa katika ngazi mbalimbali za vikao katika jamii hasa kupitia watendaji na watoa huduma ngazi ya jamii huku akieleza mikakati ya kuboresha utekelezaji wa mkataba wa lishe katika ngazi mbalimbali ambapo Idara za Afya, Elimu Msingi na Sekondari pamoja na Watendaji wa Kata wameendelea kuhakikisha utekelezaji mzuri wa viashiria vyote vya lishe katika ngazi mbalimbali pamoja na kuendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa lishe bora hususani kwa wanawake walio katika umri wa kuzaa na wajawazito.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.