Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam Mhe. Omary Kumbilamoto amefungua rasmi Mashindano ya Tigopesa Bodaboda Mbungi ya Kishua 2023 yenye kauli mbiu isemayo ‘Timiza wajibu dai haki yako’ ufunguzi uliofanyika kwenye uwanja wa Kampala uliopo Gongolamboto Jijini Dar es Salaam.
Mashindano hayo yaliyoyopo hatua ya awali ya kutafuta timu 15 yanajumuisha Wilaya tano za Ilala, Temeke, Kinondoni, Kigamboni pamoja na Ubungo ambapo kila Wilaya inatakiwa kuwa na timu tatu ambazo zitaenda kushiriki hadi hatua ya fainali, aidha kwa Wilaya ya Ilala timu 19 zimeweza kujisajili ili kuweza kushiriki katika hatua hii ya awali ya kutafuta timu 3. Aidha, wakati wa ufunguzi wa mashindano hayo, Mstahiki Meya amewaasa wanamichezo hao kucheza kwa bidii kwani michezo inatoa fursa mbalimbali hivyo amewataka waendesha pikipiki kuthamini soka.
“Mashindano haya yamekua chachu ya kupenda michezo kwani hii inaonesha juhudi kubwa za Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muunganowa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha Sekta ya Sanaa na Michezo inakua kwa kasi Nchini hivyo niwasihi sana muendelee kuthamini soka kwani michezo ni Afya na ajira kwa ujumla. Pia nipende kutoa shukrani zangu kwa Kampuni ya Tigo kwa Kudhamini mashindano haya ambayo yameonekana kufanikiwa kwa kiasi kikubwa jambo ambalo limeongeza hamasa katika michezo hivyo niwahakikishie kushirikiana nanyi bega kwa bega Mpaka mwisho wa Mashindano haya" amesema Mhe. Kumbilamoto
Kwa upande wake Katibu wa Chama cha Madereva na wamiliki Pikipiki Mkoa wa DSM (CMPD) Bw. Daudi Laurian ameeleza kuwa Mashindano Haya yaliyoandaliwa na Chama Cha Bodaboda Mkoa wa Dar es Salaam(CMPD) kwa udhamini wa Tigo yalianza rasmi tarehe 16 na 17 katika Wilaya ya Kigamboni na yanafanyika kwa Wilaya zote za Mkoa wa Dar es Salaam lengo likiwa ni kutafuta timu 15 zitakazoweza kushiriki katika Mashindano haya kuanzia hatua ya mchuano Mpaka hatua ya fainali zinazotarajiwa kufanyika Oktoba ambapo mshindi wa kwanza atapewa fedha taslimu shilingi milioni 10 huku mshindi wa pili akipata milioni 5 na mshindi wa tatu kupokea shilingi Milioni 3.
Aidha Bw. Laurian ameendelea kusema “Mashindano haya ni bure kwa Bodaboda wote ambao wana vituo vya kuegesha(vijiwe) na yana lengo la kujumuisha madereva mbalimbali wa Bodaboda na bajaji pamoja na kuibua vipaji vya mpira kwenye vituo vyetu huku tukihakikisha tunawapa elimu juu ya kujiunga na chama cha Bodaboda kwa fursa zaidi.”
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.