Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Albert Chalamila leo Julai 10, 2024 amefanya kikao na viongozi wa wafanyabiashara pamoja na viongozi wa Serikali, Taasisi, Mashirika na wataalam kutoka ofisi yake, katika ukumbi wa Arnatoglou Mnazi mmoja Wilaya ya Ilala Jijini humo.
RC Chalamila amesema Soko la Kariakoo ni Soko la Kimataifa na Serikali imefanya na inaendelea kufanya uwekezaji mkubwa, ambapo ujenzi na ukarabati wa Soko la Kariakoo kwa gharama ya zaidi ya Bilioni 28 ni moja ya ushaidi tosha wa uwekezaji huo.
Aidha, RC Chalamila ameagiza kufanyika kwa yafuatayo: mosi kuanza kupendezesha Soko la Kariakoo, kuweka mazingira yanayovutia ikiwemo kuwapanga vizuri wafanyabiashara hususani wadogowadogo, pia usafi wa mazingira unaoendana na kuweka vizuri mifumo ya maji taka na usafi kwa ujamla wake ambapo amesema wakandarasi wenye uwezo na vifaa vya kisasa ndiyo wanatakiwa.
Vilevile, DART ambaye ni msimamizi wa huduma za mabasi ya haraka kuweka mkakati kabambe wa kuhakikisha mabasi hayalali yanafanya kazi saa 24, na kuitaka Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kuangalia ruti za mabasi yanayo ingia na kutoka ukanda wa Kariakoo.
Sanjari na hilo, RC Chalamila amezitaka taasisi na mashirika katika Mkoa wa DSM kuchangia taa za barabarani ili kuwezesha usalama nyakati zote, pia kufungwa kamera za ulini (CCTV Cameras) pamoja na kuvitaka vyombo vya dola kijipanga vizuri kuimarisha ulinzi na usalama saa 24.
Sambamba hilo, Mhe. Mkuu wa Mkoa ameagiza Uhamiaji kufanyia kazi wafanyabiashara wa kigeni wanaojishughulisha na kazi ambazo zingeweza kufanywa na wazawa, vilevile taasisi za fedha kuanza kujipanga kuwa na dirisha la kutoa huduma hiyo saa 24 vilevile TANROADS na TARURA kuhakikisha barabara za ukanda wa soko la kariakoo zinakuwa nzuri bila mashimo.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Edward Mpogolo amemuhakikishia Mkuu wa Mkoa kusimamia kwa weledi mkubwa maelekezo yake kwa masilahi mapana ya Mkoa na Taifa kwa ujumla.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.