Balozi wa Jamhuri ya Korea Kusini nchini Tanzania Mhe. Eunju Ahn ametembelea Hospitali ya Mama na Mtoto iliyopo Chanika ambapo amepokelewa na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Jerry Silaa ikiwa ni sehemu ya mwaliko wa kutembelea na kukagua maendeleo ya Hospitali hiyo.
Awali akiongea mbele ya Balozi huyo mara baada ya kuwasilisha taarifa ya Hospitali, Mhe. Waziri Silaa ambaye pia ni mbunge wa Jimbo la Ukonga amesema mbali na mafanikio yaliyopatikana ambayo kwa namna kubwa yanawanufaisha wananchi wa Chanika, Ukonga kwa ujumla pamoja na wilaya za jirani amemuomba Balozi Ahn kusaidia upanuzi wa huduma ikiwa ni sambamba na ujenzi wa jengo la wagonjwa wa dharura pamoja na wagonjwa wa nje ili kuongeza wigo wa utoaji huduma kwa wananchi.
Naye Balozi wa Korea Kusini nchini Tanzania Mhe. Eunje Ahn ameahidi kuyafanyia kazi maombi hayo kupitia KOICA huku akimtoa wasiwasi Mhe. Waziri na Mbunge wa Jimbo la Ukonga Jerry Silaa.
"Nitayachukua niliyoyaona na kuyasikia kutoka kwenu na kufikisha ujumbe huu kwa Serikali yangu, na nafikiri aina hii ya miradi inachukua muda lakini kipekee nampongeza Waziri kwa mapenzi yake kwa wananchi na jimbo lake kwa ujumla." amesema Balozi Ahn.
Katika hatua nyingine, Mhe. Waziri Jerry Silaa amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna anavyowajali wananchi wa Ukonga kwa kuwasogezea karibu huduma mbalimbali za maendeleo hususan huduma ya Afya.
Hospitali ya Chanika inatoa huduma kwa zaidi ya wakazi 188,633 huku upatikanaji wa dawa ukiwa ni 99% ambapo imefanikiwa Kupunguza vifo vya uzazi kutoka 3 mwaka 2022 had kifo 1 mwaka 2023 na 2024.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.