Waheshimiwa Madiwani na wajumbe wa Baraza la Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam wamepatiwa mafunzo elekezi ya namna ya kusimamia sheria, kanuni na taratibu katika utekelezaji wa miradi kwa ajili ya utoaji wa huduma bora na maendeleo kwa wananchi.
Mafunzo hayo ya siku mbili yenye lengo la kuwajengea uwezo Waheshimiwa Madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam yamefunguliwa leo tarehe 07 Januari, 2021 katika ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam na Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam ndugu Paulo Makanza, ambaye alikua ni mgeni rasmi.
Akifungua mafunzo hayo elekezi, ndugu Makanza ametoa wito kwa Waheshimiwa Madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kushiriki kikamilifu katika mafunzo na kuyaelewa ili kuwa na uwezo wa kufanya maamuzi sahihi, kuweza kuyasimamia, kuleta ufanisi, ustawi na tija kwa Jiji la Dar es Salaam.
“Naomba tuchukulie kila kitu kwa uzito zaidi, mapana zaidi na marefu zaidi ili tukimalize muda wa uongozi wetu tuache alama chanya”, Alisema Makanza.
Mafunzo hayo yalitolewa na wataalam kutoka taasisi mbalimbali za Serikali zikiwemo Chuo cha Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma ambapo mada mbalimbali zikihusisha Historia na uhalali wa Mamlaka za Serikali za Mitaa, Uongozi na Utawala Bora, Maadili ya Madiwani, Usimamizi wa Fedha katika Mamlaka za Serikali za Mitaa, Ufuatiliaji, Usimamizi na Uchambuzi wa Taarifa za Fedha na Ukaguzi, Usimamizi wa Mpango, Bajeti, Miradi na Utambuzi wa Vipaumbele vya Halmashauri na vya Kitaifa ziliwasilishwa kwa Waheshimiwa Madiwani.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.