Katika kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya Mwaka 2020 hadi 2025 leo Machi 16,2023 Halmashauri kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ilala wamefanya Mkutano wa kujadili utekelezaji wa miradi iliyotekelezwa na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kuanzia Januari 2021 hadi Disemba 2022.
Mkutano huo uliofanyika katika Ukumbi wa Arnatouglou Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam na uliweza kuhudhuriwa na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Ilala, Katibu wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Ilala, Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Ilala, Wajumbe wa Halmashauri kuu Wilaya ya Ilala pamoja na Watumishi kutoka Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.
Akizungumza katika Mkutano huo Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Ilala Ndg. Said Sidde amesema “Niwapongeze Wajumbe wa Halmashauri kuu kwa kupokea na kupitisha Utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) pia nipende kuipongeza Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa kutekeleza Ilani ya chama kwani wameweza kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwa kuboresha huduma za wananchi ila niwaombe viongozi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kuhakikisha mnatekeleza yale yote tuliyowaelekeza wakati wa ziara yetu na pia muhakikishe miradi yote inatekelezwa kwa wakati uliopangwa”.
Kwa upande wake Naibu Spika wa Bunge ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Ilala Mhe. Mussa Azzan Zungu amesema “Nawashukuru sana wilaya ya Ilala kwa kuwa Wahamasishaji wazuri kwani Kata zote 36 zimeweza kupata hamasa juu ya utekelezaji wa Ilani ya chama cha Mapinduzi, mmelifurahisha Taifa pamoja na Mheshimiwa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwani mmekua mkitekeleza majukumu ya Kamati Kuu hadi kuwadhamini wajumbe wa shirika”.
Akiwasilisha taarifa ya Utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Katibu Tawala wa Wilaya ya Ilala Bi. Charangwa Selemani ameeleza kuwa “Katika kutekeleza ilani ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imeweza kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika Idara zake zikiwemo Idara ya Elimu, Idara ya Afya, Idara ya Maendeleo ya Jamii pamoja na Idara ya Maliasili na Mazingira ambapo katika Idara ya Elimu Msingi na Sekondari Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imeendelea kupokea Fedha kwa ajili ya kuboresha Elimu ya Msingi ambapo asilimia 40% ya fedha hizo zinanunulia vitabu, huku fedha zinazopokelewa shuleni ni asilimia 60% ambapo asilimia 30% inanunua vifaa vya kufundishia ambavyo siyo vitabu, asilimia 30% hutumika katika ukarabati wa miundombinu huku asilia 20 % zikitumika kwenye mitihani, asilimia 10% zikitumika kwa ajili ya UMITASHUMTA na 10% Utawala. Pia kwa upande wa kuboresha Elimu ya Sekondari tuliweza kupokea shilingi bilioni 5.1 kwa mwaka 2021 zikiwa ni fedha za Uviko 19 ambazo zilitumika kujenga madarasa 255 na yote yalikua madarasa ya msambao huku mwaka 2022 Halmashauri ilipokea kiasi cha shilingi bilion 6.2 kutoka Pochi la Mama ambazo zilitumika kujenga madarasa 310 huku 37 yakiwa ya ghorofa”.
Kwa upande wa kuboresha huduma za Afya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imeendelea kutoa huduma mbalimbali za afya kupitia vituo vyake vya Afya huku elimu ya afya ikiendelea kutolewa kwa Wananchi.
Aidha Bi. Charangwa ameendelea kusema Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kupitia Idara ya Maendeleo ya Jamii imefanya uhamasishaji wa kutoa mikopo kwa Vijana, Wanawake na Watu wenye Ulemavu kwa pesa za asili 10% za mapato ya ndani ya Halmashauri ambapo kiasi cha shilingi bilioni 3.6 zilitolewa kwa vikundi 316 vya vijana huku idara ikiendelea kutoa elimu ya ujasiriamali , elimu rika , afya ya uzazi na stadi za maisha pamoja na kutoa mikopo isiyo na riba kwa vikundi 418 vya wanawake katika kata 36 za Halmshauri ya Jiji la Dar es Salaam.
Vilevile Bi.Charangwa ameendelea kusema “Katika uboreshaji wa Mazingira Halmashauri imekua ikisimamia usafi wa mazingira kwa kuwasimamia Wakandarasi na Vikundi vya uzoaji Taka pia tumekua tukifanya usafi kila Jumamosi ya mwisho wa Mwezi hivyo nitoe wito kwa Wajumbe Halmashauri Kuu mjitokeze katika Kata zenu kufanya usafi na pia muwahimize Wananchi wa Kata zenu kuweka Mazingira katika hali ya usafi lengo likiwa ni kuhakikisha Jiji letu linakua katika hali ya usafi”.
Sambamba na hilo Bi.Charangwa ameendelea kusema “Hakuna jambo tunalolifanya ambalo haliko kwenye kitabu cha Ilani kwani Ilani ndo Dira pekee ya kutuongoza katika utekelezaji wa miradi yote ya maendeleo hivyo naomba tuzingatie kitabu cha ilani katika utekelezaji wa miradi yetu ya maendeleo kwa kwa lengo la kutoa huduma kwa wananchi."
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.