Wakazi wa Jiji la Dar es Salaam imehimizwa kupanda miyi kwa wingi pamoja na kuacha kutupa taka ovyo lengo likiwa ni kupendezesha Jiji pamoja na kujikinga na magonjwa ya mlipuko kama Kipindupindu.
Wito huo umetolewa na Afisa Tawala wa Wilaya ya Ilala Flora Mgonja kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Ilala wakati aliposhiriki katika Mdahalo wa utoaji elimu kuhusu utunzaji wa mazingira leo Juni 3, 2024 katika Ukimbi wa Karimjee Jijini humo ikiwa ni muendelezo wa matukio yanayofanywa na Jiji la Dar es Salaam katika kuelekea siku ya Mazingira Duniani ambayo huadhimishwa Juni 5 ya kila Mwaka ikiambatana na kauli mbiu isemayo ‘Urejeshwaji wa Ardhi, Ustahimilivu wa hali ya Jangwa na ukame’
Akizungumza na Wadau, Wanafunzi, watumishi kutoka Jiji la Dar es Salaam pamoja na wananchi wote walioshiriki katika mdahalo huo Bi. Mgonja Amesema “Pamoja na Serikali kuboresha huduma za afya ila suala la utunzaji wa mazingira na usafi ni wakila mmoja hivyo tuwajibike katika kutunza mazingira yetu kila mmoja awe balozi wa Mwenzake, mdahalo huu uwe endelevu tusisubiri hadi wiki ya mazingira ndo tuanze kufanya midahalo ya mazingira inabidi muweke mashindano katika ngazi za Kata ili kuhamasisha Wananchi kupanda miti na kutunza mazingira pia napenda kulipongeza Jiji la Dar es Salaam kwa kuhakikisha mnaboresha mazingira ya Jiji letu kwa kupanda miti, kuweka perving pamoja na kuhamasisha zoezi la usafi kila mwezi kwa wananchi”.
Aidha, Bi. Mgonja ameendelea kusema Kaulimbiu ya Madhimisho ya siku ya Mazingira duniani inaakisi suala zima la upandaji miti na hivyo kutoa wito kwa Wananchi kupanda miti kwa wingi ili kupendezesha Jiji pamoja na kukabiliana na athari za Kimazingira.
Halikadhalika, Bi. Mgonja amewataka Wadau wa Mazingira washirikiane na Serikali kuhakikisha wanatunza mazingira kwa kuwa mabalozi wa kulinda mazingira na kuhakikisha hawatupi taka ovyo.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam Tabu Shaibu ameeleza kuwa kama sehemu ya maadhimisho ya Mazingira Duani, Jiji la Dar es Salam limefanya shughuli mbalimbali za kuelimisha na kuhamasisha jamii kuhusu utunzaji wa mazingira pamoja na utupaji taka holela huku akiahidi kampeni hii ya usafi kuwa desturi kwa wananchi wa Ilala ili kuboresha mazingira kwa afya na ustawi wa wananchi hao.
Aidha wadau Mbalimbali waliochangia mada katika mdahalo huo waliweza kuhimiza suala la elimu, uzalendo na nidhamu kwa wananchi katika utunzaji wa mazingira.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.