Na; Judith Msuya.
Wakuu wa Shule za Sekondari za Umma pamoja na za Binafsi za Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam leo Augusti 21, 2021 wamefanya kikao kazi kwa ajili ya maandalilizi ya kuwapokea wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka 2022, kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa Shule ya Sekondari ya Shaabani Robert Jijini Dar es Salaam kimehudhuriwa pia na Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Maafisa Elimu kata pamoja na mafundi ujenzi wanaotumika kujenga Shule mbalimbali.
Akizungumza katika kikao kazi hicho Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Ng'wilabuzu Ludigija amesema kuwa wanafunzi takribani 28,480 wanatarajiwa kufanya mtihani wa darasa la saba mwaka huu ambapo makadirio ya wanafunzi watakao faulu wanatarajiwa kuwa Wanafunzi 26,800 ambao ni idadi kubwa na wanatakiwa kuingia darasani kwa wakati hivyo maandalizi lazima yafanyike mapema ili ifikapo Januari 2022 Wanafunzi wote watakaofaulu waweze kuingia darasani kwa wakati.
"Tumetenga fedha takribani milioni 900 kwaajili ya kuongeza madarasa na kununua vifaa vya shule Kwa baadhi ya Shule kwa ajili ya Wanafunzi watakao faulu kuingia kidato cha kwanza 2022 hivyo fedha hizo zitatolewa mapema ili taratibu za utekelezaji zianze kusudi tuweze kuepusha usumbufu uliojitokeza mwaka 2021 ambapo Wanafunzi walichelewa kuanza masomo kwa wakati muafaka kutokana na ujenzi kuchelewa kukamilika". alisema Mhe. Ludigija.
Sambamba na hilo Mkuu wa Wilaya amewasisitiza Wakuu wa Shule hao kuhakikisha wanatunza nyaraka zote za malipo ya Miradi, barua za vikao pamoja na nyaraka zote za muhtasari wa vikao vyao zinahifadhiwa vizuri kwa ajili ya kumbukumbu za badaye bila kusahau kuwashirikisha wananchi wanaowazunguka kwani pamoja na kwamba fedha zinatolewa na Serikali lakini miradi hiyo inawahusu Wananchi hivyo sibudi kuwashirikisha Wananchi hao ili kufanya mambo kuwa mepesi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya ujenzi wa shule.
Kwa upande mwingine Mhe. Ludigija aliwapongeza Wakuu wa Shule kwa ushirikiano mzuri baina yao na viongozi wao kutoka ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa kazi kubwa waliyoifanya kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2021 kwa kujenga madarasa takribani 178 kwa muda mfupi na hivyo kuwaagiza Wakuu wa shule kuhakikisha kuwa kuelekea kipindi hiki cha mitihani wahakikishe wanafunzi wote wamesajiliwa kama inavyotakiwa ili kuepusha usumbufu unaojitokeza kwa wanafunzi na Wazazi katika kipindi cha mitihani.
"Nawashukuru sana kwa mchango wenu na nawaahidi kushirikiana na nyinyi katika utekelezaji wa miundombinu, kudumisha michezo, nidhamu pamoja na taaluma katika shule zetu ili kuhakikisha Halmashauri yetu ya Jiji la Dar es Salaam inakua kinara katika kuboresha Elimu na Pia niwaombe 'local Fundi' unapopata kazi kwenye Jiji la Dar es Salaam unaikamilisha kwa wakati ili kuepusha usumbufu kwa Walimu wakuu wa Shule ambao wanasimamia Taaluma kwa watoto wetu."
Kikao kazi hicho kilicho funguliwa na Afisa Elimu Mkoa wa Dar es Salaam Ndug.Abdul Maulid ambaye amewasisitiza Wakuu wa Shule za Sekondari za Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam kuhakikisha wanasimamia shule katika misingi ya kisheria, taratibu na kanuni katika kusimamia nidhamu ya Shule, usafi wa mazingira, ulinzi na usalama, michezo na burudani pamoja na kuhakikisha wanasimamia vyema miundombinu ya Shule ili kuhakikisha fedha zinazotolewa na Serikali kwenye 'Force Account' kwa lengo la kuboresha miundombinu ya shule zinatumika vyema ili kuhakikisha ujenzi bora wa majengo ya shule unakamilika kwa wakati na unatekelezwa kwa kiwango cha hali ya juu.
Aidha, kikao hicho kilifikia tamati kwa Wakuu wa Shule kuweza kutoa maoni yao na kuahidi kuwa watatekeleza yote waliyoagizwa kuyafanya ikiwemo suala zima la usimamizi wa miundombinu ya Shule na Taalumu kwa ujumla.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.