Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam leo tarehe 19 Januari, 2024 imefanya kikao cha dharura na Walimu wa Masomo ya Afya wa Shule za Msingi na Sekondari za Serikali na binafsi zilizopo ndani ya Halmashauri hiyo kujadili juu ya kuenea na kusambaa kwa ugonjwa wa mlipuko wa macho (Red Eyes) kilichofanyika katika ukumbi wa Arnatoglou.
Akiongea na Walimu walioshiriki kwenye kikao hicho, Mratibu wa Magonjwa ya Mlipuko Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam Ndg. Michael Gweba amewasisitiza walimu kutoa elimu kwa wanafunzi na jamii kwa ujumla kutotumia njia mbadala za kutibu ugonjwa huo na wagonjwa kupelekwa hospitali kwa matibabu zaidi.
"Walimu hakikisheni mnawapa ruhusa ya kukaa nyumbani wanafunzi wenye maambukizi ya ugonjwa wa macho au wenye dalili za ugonjwa huo ili wasiweze kuusambaza kwa wanafunzi wengine." Amesisitiza Ndg. Gweba.
Aidha, Mratibu wa Afya ya Macho Anne Kisoka amesema ”Tumewaita walimu wa Afya kwa sababu walimu ndio mabalozi kwenye jamii zetu. Mwalimu akipata elimu atamfundisha mwanafunzi na mwanafunzi atamfundisha mzazi/mlezi. Lakini pia maambukizi mengi yapo mashuleni kutokana na muingiliano mkubwa wa wanafunzi. Hivyo kwa kutoa elimu hii kwa walimu na wao kuishusha kwa wanafunzi tunaamini itasaidia kupunguza maambukizi kwa kiasi kikubwa."
Sambamba na hilo Bi. Anne amesema ili kuepukana na ugonjwa huo, ni muhimu kunawa mikono mara kwa mara kwa maji tiririka na sabuni, kutumia vitakasa mikono, kuosha macho kwa maji baridi, kuepuka kunawa kwa maji yenye chumvi, au kutumia njia mbadala kama kuweka vitunguu swamu kwenye macho kwani vinaweza kusababia uoni hafifu.
Hata hivyo Kaimu Afisa Lishe wa Halmashauri hiyo Bi. Neema Mwakasege amesema “Ugonjwa unaendana na kinga za mwili hivyo tujitahidi kula mlo kamili unaotokana na makundi ya vyakula ili miili iweze kujenga kinga imara zinazoweza kupambana na magonjwa mbalimbali.”
Akiongea kwa niaba ya walimu, Mwl. Catarina Christopher wa shule ya Msingi Buguruni ameishukuru Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa elimu waliyoipata na kuahidi kuwa mabalozi wazuri wa kuelekeza yale yanayopaswa kufanywa na yasiyopaswa kufanya ili kuzuia ugonjwa huo kuenea mashuleni na katika jamii kwa ujumla.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.