Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amewataka wajasiriamali kujiunga na majukwaa ya wanawake lengo likiwa ni kurasimisha biashara zao ili waweze kufanya biashara kwa wigo mpana zaidi.
Mhe. Dkt. Gwajima ameyasema hayo tarehe 11 Septemba, 2023 katika ufunguzi wa Maonesho ya Wajasiriamali yaliyoandaliwa na Taasisi ya CRDB Bank kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya Ya Ilala yenye kauli mbiu isemayo ‘Asante Rais Samia biashara zimefunguka’ lengo likiwa ni kutoa muamko kwa wajasiriamali ili waweze kuchangamkia fursa mbalimbali zinazopatikana baada ya kujiunga na majukwaa mbalimbali yanayoambatana na elimu ya ujasiriamali.
Aidha Dkt. Gwajima ameongeza kuwa ili kwenda na wakati na kupata fursa zinazotokea katika mchakato mzima wa ununuzi ni vyema wajasiriamali wakarasimisha biashara zao na kujiunga na majukwaa ya wanawake kwani Sekta binafsi zinaonesha mchango mkubwa wa kuwakwamua wanawake na vijana ili kukuza uchumi wa taifa letu.
“Nipende kumshukuru Raisi wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzanzia Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuamua kuunda Wizara hii ili ishirikiane na ninyi kwani kuna faida nyingi kwenye majukwaa hivyo wanawake mnyanyuane mfike kwenye majukwaa fursa zipo muachane na mikopo yenye riba kubwa nendeni ‘Imbeju’ kuna fursa.” Ameeleza Dkt. Gwajima.
Vilevile Dkt. Gwajima ametoa shukrani zake kwa CRDB Bank na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ilala kwa kuanzisha maonesho haya endelevu huku akiahidi kuitangaza programu yao ya ‘imbeju’ wakati anapokua kwenye mikutano yake mbalimbali lengo likiwa ni kuhakikisha wajasiriamali wote wanapata elimu za kuboresha bidhaa zao na kupata masoko zaidi.
Akiongea kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Edward Mpogolo ameeleza kuwa “Katika kuwawezesha wananchi kiuchumi, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ilala kupitia Idara ya Maendeleo ya Jamii tulishirikiana na CRDB Bank ambapo walitueleza juu ya Programu ya Imbeju huku na sisi tukiwa na Asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri hivyo tuliona ni vyema kuungana kuanziasha maonesho haya lengo likiwa ni kutengeneza masoko kwa wajasiriamali wetu na kuwapa elimu juu ya ujasiriamali. Hivyo tunawashukuru sana CRDB Bank foundation kwa kuanzisha programu ya Imbeju ambayo imekua chachu ya wajasiriamali kujipatia mikopo mbalimbali kwaajili ya kuendeleza biashara zao na kujikwamua kiuchumi.”
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Ndg. Abdulmajid Mussa Nsekela ameleza kuwa katika kuwakwamua wanawake na vijana Wajasiriamali elfu 65 wamefikiwa na programu ya imbeju huku mikopo ya zaidi ya shilingi Milion 200 zikitolewa kwa baadhi ya vikundi vya wajasiriamali.
Aidha katika maonesho hayo mikopo mbalimbali ilikabidhiwa kwa baadhi ya wajasiriamali ikiwepo mikopo ya bajaji, pikipiki pamoja na fedha taslimu.
Maonesho haya ni bure na yatafanyika kwa siku tatu kuanzia leo tarehe 11 hadi 13 ambapo wananchi watapewa elimu mbalimbali juu ya ujasiriamali na jinsi ya kutafuta masoko ndani ya nchi na nje ya nchi.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.