Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Mohamed Mchengerwa leo Septemba 2, 2024 amezindua Kadi Janja na Mageti janja kwa ajili ya kununua na kuhakiki tiketi za usafiri wa Mabasi Yaendayo Haraka.
Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi huo uliofanyika katika Kituo Kikuu cha Kimara, Mhe. Mchengerwa ameupongeza Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) kwa kutekeleza maelekezo ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Kamati ya Bunge kuhusu kuachana na tiketi za Karatasi.
“Dhamira ya Mheshimiwa Rais ni kuhakikisha tumeboresha usafiri wa Umma katika Jiji la Dar es Salaam kwa kumaliza changamoto zote za abiria kabla ya kwenda kwenye mikoa mingine” Amesema Mhe. Mchengerwa.
Aidha, Mhe. Mchengerwa amesisitiza watumishi wa DART pamoja na watoa huduma wake kuhakikisha wanafanya kazi kwa ushirikiano katika kutoa huduma bora kwa wananchi na kujibu hoja za abiria kwenye Mradi wa DART.
Mhe. Mchengerwa ameongeza kuwa mbali na kuwarahishia abiria kusafiri kwa wakati pia matumizi ya Kadi pamoja na mageti janja vitasaidia mradi kati katika utunzaji wa mazingira.
“Mfumo huu uliojengwa na Wataalam wa Mabasi Yaendayo Haraka una faida nyingi ikiwemo kuondoa uchafuzi wa mazingira, zitasaidia kuondoa usumbufu wa chenji pia kuondoa foleni za kununua tiketi, pia kadi hizi zina ubora ukilinganisha na nyingine zinazotumika huko”.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wizara kwa Wakala wa DART, Dkt. Florens Turuka amesema kwa DART ni jambo la fahari kuona mifumo inaimarika kwenye kuendesha usafiri wa Mabasi Yaendayo Haraka na dhamira yao ni kuona kuwa mifumo hii inarahisisha na kuleta tija Jijini Dar es Salaam.
Kadi na Mageti janja yaliyozinduliwa yanayotokana na Mfumo wa Serikali wa Ukusanyaji nauli (AFCS) ni juhudi za serikali katika kutumia wataalam wa ndani kuunda mifumo itakayotoa suluhu ya changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi katika kuzifikia huduma.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.