Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Adolf Mkenda ametoa pongezi kwa watendaji wa baraza la mitihani la Tanzania ( NECTA) kwa kufanya kazi kwa weledi pamoja na kusimama madhubuti kwa miaka 50 kutatua changamoto mbalimbali zinazotokea ikiwa ni pamoja na kupambana na rushwa.
Prof. Mkenda ameyasema hayo Novemba 30, 2023 katika viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam wakati akifungua maadhimisho ya miaka 50 ya Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) yaliyoambatana na kauli mbiu isemayo ‘Upimaji wa umahiri kwa Misingi ya haki suluhisho la ajira katika Karne ya 21’
Akiendelea kuzungumza wakati wa maadhimisho hayo Prof. Mkenda amesema “Baraza la Mitihani la Tanzania lilianzishwa rasmi mwaka 1973 na mpaka sasa limetimiza miaka 50 hivyo nipende kuwapongeza watendaji wa NECTA kwa kusimamia vyema baraza hili ndani ya miaka 50 kwani mmeweza kufanya kazi kwa uadilifu kwa kuhakikisha mnapambana na rushwa wanafunzi wanafaulu bila udanganyifu hivyo kwakutambua mchango wenu kwenye kuboresha sekta ya Elimu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amezidi kutoa kipaumbele kwenye sekta ya elimu ambapo amehakikisha kila mtoto anapewa fursa ya kusoma hata hivyo katika kutekeleza hayo sisi kama Wizara tumeanza kushirikiana na vyuo vikuu na tutafungua matawi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika mikoa ya Tanga Kagera na Ruvuma ambayo yatakua chachu kwa wanafunzi ambao wanashindwa kusoma Dar es Salaam kwaajili ya umbali na gharama za maisha.”
Sambamba na hayo Prof. Mkenda ameeleza kuwa Serikali imeendelea kuboresha sekta ya elimu kwani wameanza kujenga Shule za Sekondari za Sayansi za Wasichana kwa kila Mkoa huku wakiendelea kutoa kipaumbele kwa Wanafunzi wenye mahitaji maalumu kwa kugawa vifaa wezeshi vya kujifunzia kwa wanafunzi hao kama vitabu vya nukta nundu pia Serikali imejenga Shule Jumuishi kwaajili ya watoto wote wenye mahitaji maalumu hivyo ametoa wito kwa wazazi kutoficha watoto walemavu nyumbani kwani kila mtoto anahaki ya kupata elimu na ukizimgatia elimu kwa sasa ni bure.
Aidha, Akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Mhe. Hashim Abdallah Komba amemuhakikishia Mheshimiwa Waziri kufanya kazi kwa ushirikiano na NECTA ili kuhakikisha wanadhibiti udanganyifu na kila mwanafunzi anapimwa katika uimara wake.
Awali akitoa taarifa kwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) Dkt. Said Mohammed ameeleza kuwa NECTA imekua ikitatua changamoto mbalimbali za wanafunzi kwa kuhakikisha hakuna udanganyifu na kwa sasa suala la kupata vyeti limeboreshwa kwani baada ya matokeo kutoka vyeti vinachukua miezi 3 tu.
Sambamba na hilo Dkt. Mohammed ameeleza kuwa “katika kuadhimisha maadhimisho hayo baraza litafanya kazi mbalimbali ikiwemo Kupanda miti katika shule za msingi na sekondari nchi nzima, zoezi lilianza mwezi Oktoba na linatarajia kukamilika mwezi Desemba 2023,Kuendesha mafunzo kwa walimu wa Taaluma kuhusu Utunzi wa maswali yanayopima umahiri na mada zenye changamoto ya ujifunzaji. Baraza liliendesha mafunzo kuanzia tarehe 9 Novemba 2023 hadi tarehe 10 Novemba, 2023 kwa walimu wa Taaluma 180 wa shule za msingi na sekondari ambapo Walimu hao waliteuliwa katika Halmashauri za Mkoa wa Tanga, Kongamano la Kitaaluma lililofanyika Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kuanzia tarehe 27 Novemba, 2023 hadi tarehe 28 Novemba, 2023, Uandishi wa Kitabu cha Historia ya Baraza la Mitihani la Tanzania (1973-2023), Maonesho ya kazi za Baraza la Mitihani la Tanzania na Taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ambapo maonesho hayo yatafanyika kuanzia tarehe 30 Novemba, 2023 hadi tarehe 3 Desemba, 2023 katika viwanja vya Mnazi Mmoja, Ujenzi wa Mnara wa Makumbusho utakaozinduliwa tarehe 4 Desemba, 2023 pamoja na Kilele cha Maadhimisho kitakachofanyika tarehe 4 Desemba, 2023 katika Ofisi za baraza hivyo nikuhakikishie mheshimiwa Waziri kazi hizo tumefanya kwa weledi na tunaendelea kufanya bila kusahau majukumu yetu kama baraza ya kuendelea kufanya kazi kwa uadilifu na uaminifu lengo likiwa ni kupata watendaji bora hapo badae huku tukihakikisha baraza linafanya kazi kwa kutekeleza sera ya elimu iliyoboreshwa ili kukuza sekta ya elimu nchini.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.