Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na wadau wa Sekta ya Afya imepiga hatua kubwa kwenye mapambano dhidi ya ugonjwa wa malaria Nchini, hayo yamebainishwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Majaliwa Kassim Majaliwa leo Aprili 23, 2023 kwenye maadhimisho ya Siku ya Malaria Duniani ambayo Kitaifa yamefanyika Jijini Dar es Salaam katika viwanja vya Mnazi Mmoja.
“Tumepiga hatua kubwa kwenye mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Malaria, tumeweza kupunguza kiwango cha maambukizi kutoka asilimia 14.8 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 8.1 mwaka 2022." amesema Waziri Mkuu Majaliwa.
Mhe. Majaliwa amesema kauli mbiu ya maadhimisho ya siku ya malaria duniani kwa mwaka huu ambayo ni ‘Wakati wa kutokomeza Malaria ni sasa, Badilika, Wekeza, Tekeleza. Ziro Malaria inaanza na Mimi’ itekelezwa kwa vitendo kwa kuwa inaenda sambamba na utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ibara ya 83 (M,N,O) ya utekelezaji wa mkakati wa Serikali kwenye Mapambano dhidi ya Malaria.
“Ilani ya Chama Cha Mapinduzi imetoa maelekezo kwa Serikali, kuendelea kuihamasisha jamii juu ya matumizi ya vyandarua vilivyowekwa dawa, kupulizia viuwatilifu ukoko kwenye nyumba, kutekeleza mpango wa kuangamiza viluilui vya mbu na kutoa hamasa katika mapambano dhidi ya magonjwa ya kuambukiza” ameeleza Waziri Mkuu.
Aidha katika maadhimisho hayo Mhe. Majawiliwa amezindua gari maalumu litakalotumika katika shughuli mbalimbali za utafiti juu ya ugonjwa wa Malaria pamoja na Uzinduzi wa baraza la kupambana na Malaria lenye wajumbe 19 huku akiwasisitiza kuhakikisha wanafanya kampeni za kudhibiti ugonjwa huo kwa kuanza na Mikoa ambayo iko chini ya asilimia moja ili kutokomeza kabisa ugonjwa huo.
Katika kutelekeza kwa Vitendo mapambano dhidi ya ugonjwa wa malaria, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa amesema kuwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ametoa unafuu kwa watanzania kwa kupata huduma za tiba ya ugonjwa wa malaria bure, ikiwemo Vipimo vya MRDT, Dawa za Aru, Sindano ya Malaria kali, Dawa za SP kwa ajili ya kutibu Malaria kwa wajawazito vyote vitatolewa bure kuanzia sasa.
Kwa upande wake Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema Serikali imeendelea na mapambano dhidi ya kutokomeza ugonjwa huo na hadi kufikia mwaka 2022, idadi ya Mikoa yenye kiwango cha maambukizi ya malaria chini ya asilimia moja imefikia 9 (Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Dodoma, Singida, Iringa, Dar es Salaam, Songwe na Mwanza) kutoka Mikoa 6 mwaka 2017 hivyo kufanya asilimia ya watu wanaoishi katika maeneo yenye malaria chini ya asilimia moja kufikia asilimia 41.
Sambamba na hilo Mhe. Ummy amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya imeweka kipaumbele kikubwa kwenye mapambano ya kutokomeza ugonjwa wa Malaria ifikapo Mwaka 2030 hivyo ni vyema Wadau wa Sekta ya Afya kwenye mapambano dhidi ya Malaria wakaunganisha nguvu za pamoja na Serikali katika utekelezaji wa afua za mapambano dhidi ya ugonjwa huo na kuweza kuutokomeza nchini.
Akitoa Shukrani zake kwa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Amos Makalla amesema “Tunamshukuru Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutoa fedha zaidi ya bilioni 37 kwaajili ya kuboresha huduma za Afya katika Mkoa wa Dar es Salaam kwani fedha hizo zimetumika katika kujenga Zahanati, vituo vya Afya pamoja na kuboresha huduma mbalimbali katika Hospitali za Wilaya ambazo zinaendana na kasi za utokomezaji wa ugonjwa wa malaria pia tunashukuru kwani Wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam wameweza kupata elimu ya jinsi ya kujikinga na Malaria ambapo Mkoa wa Dar es Salaam umeweza kupunguza maambukizi ya ugonjwa wa malaria kwa asilimia kubwa kutoka asilimia 6% Mpaka kufikia 0.9% za maambukizi hii inatokana na kampeni ya ‘Safisha Pendezesha Dar es Salaam’ ambayo imeonesha mafanikio makubwa kwani Wananchi wamekua wakisafisha mitaro ya maji, kufyeka majani, kiziba madimbwi ya maji bila kusahau kulala kwenye chandarua hivyo naamini Mkoa wa Dar es Salaam utakua wa kwanza kutokomeza ugonjwa wa Malaria Nchini”.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.