Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa kushirikiana na Ofisi ya Kamishina msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Dar es Salaam inategemea kutoa hati zaidi ya elfu nne (4000) katika Zoezi la Ardhi Clinic lililo chini ya Mradi wa Uboreshaji na Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) unaofadhiliwa na Benki ya Dunia na kusimamiwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi .
Hayo yamebainishwa leo tarehe 14 Novemba, 2024 wakati wa zoezi la Ardhi Clinic, linalofanyika katika Shule ya Msingi Mzambarauni iliyopo Kata ya Ukonga Jijini Dar es Salaam na litadumu mpaka tarehe 27 Novemba, 2024.
Akiongea wakati wa zoezi hilo, Meneja wa Urasimishaji Mjini Bw. Leons Mwenda amesema “Lengo la Serikali kuanzisha Ardhi Clinic ni kuwapunguzia wananchi muda na umbali wa kushughulikia masuala ya Ardhi ikiwemo kutatua changamoto zote zinazohusu urasimishaji ardhi ikiwemo kupanga na kupima maeneo yanayoyohitaji leseni za makazi na hati Miliki, kurahisisha gharama za upimaji, kutoa hati na leseni za makazi pamoja na kuboresha miundombinu ya ardhi kwa nchi nzima”
Kwa upande wake Mratibu wa Ukwamuaji wa Urasimishaji Mkoa wa Dar es Salaam Bw. Paul Mbembela amesema “Kupitia zoezi hili kwa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam tunakusudia kutoa hati zaidi ya 4000 pamoja na kukwamua urasimishaji wote uliokwama, kwani tuna Wataalamu wa Ardhi kutoka Halmashauri yetu na wanafanya kazi usiku na mchana".
Aidha, Bw. Mbembela ametoa wito kwa wananchi wenye changamoto mbalimbali za Ardhi kujitokeza kwa wingi katika Zoezi hilo Ili waweze kuonana na wataalamu na kupatiwa ufumbuzi.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.