Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mh. Amos Makalla, amewaagiza wasimamizi na mkandarasi katika machinjio ya kisasa ya Vingunguti kusimamia kwa umakini ukamilishaji wa machinjio hiyo. Mheshimiwa Makalla ameagiza hivyo alipofanya ziara katika machinjio hiyo leo Juni 9, 2022.
“Namshukuru Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Samia Suluhu Hassan kwa fedha nyingi alizozitoa katika ujenzi wa machinjio ya Vingunguti. Hivyo naomba ujenzi wa machinjio hayo ukamilike kwa muda uliopangwa. Ni matarajio yangu kwamba kwamba mkandrasi atafanya kazi usiku na mchana kukamilisha ujenzi ili tuanze kufanya biashara ya kuuza nyama kimataifa”.
Mkuu huyo wa Mkoa, alikagua kazi iliyokwisha fanya na kuelekeza kwamba vyumba vya kuhifadhia nyama kwa ajili ya biashara kimataifa, ujenzi wa tanki la maji, maeneo ya kuwekea mbolea vikamilishwe haraka. Aidha, aliwataka wafanyabiashara ya nyama katika machinjio hiyo kutambua hadhi ya machinjio ya vingunguti ambayo itakidhi malengo ya biashara kutokana na uwezo mkubwa wa machinjio. Katika machinjio hiyo ng’ombe wapatao elfu moja na mbuzi mia tano wanaweza kujichwa kwa wakati mmoja.
Aliwataka wafanya biashara hao kubadilika na kuzitumia vema fursa zinazotokana na machinjio hiyo. “Wafanyabiashara mbadilike, mfanye biashara kuendana na machinjio hii ya kisasa ikiwa na mazingira mazuri ya utendaji kazi. Acheni kufanya kazi kwa mazoea tunatakiwa kubadilika na kufanya kazi katika mabucha hayo ya kisasa,” alisema Mheshimiwa Makalla.
Kupitia ziara hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mh. Ng’wilabuzu Ludigija, alimshukuru Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa kufanya ziara hiyo. “Nashukuru ujio wako Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa katika machinjio yetu ya Vingunguti. Umefanya ziara katika machinjio hii mara kwa mara kuona nini kinaendelea na kwa kiasi kikubwa tumepambana kuhakikisha mabucha ya sehemu ya machinjio hii yanakamilika kwa mujibu wa makubaliano tuliyofikikia ili wafanyabiashara waweze kuhamia katika machinjio hii mpya,” alisema Mheshimiwa Ludigija.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.