Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mheshimiwa William Lukuvi (Mb) leo tarehe 27 Julai, 2018 amezindua utoaji wa mapendekezo au maoni ya Rasimu ya mwisho ya Mpango Kabambe "Master Plan" wa Jiji la Dar es Salaam utakaotumika kwa kipindi cha miaka 20 ijayo.
Akizungumza mbele ya viongozi mbalimbali wa dini na Serikali, wananchi pamoja na wadau mbalimbali wa Jiji la Dar es Salaam, Waziri Lukuvi ameeleza kwamba uzinduzi huu wa mawasilisho ya utoaji maoni ya Rasimu ya Mpango Kabambe wa Jiji la Dar es Salaam utawawezesha wananchi na wadau mbalimbali wa Jiji la Dar es Salaam kuwasilisha maoni na mapendekezo yao na kuwezesha kuwa na Mpango Kabambe shirikishi kwa ajili ya maendeleo endelevu ya Jiji la Dar es Salaam.
Aidha amewasihi wakazi wa Jiji la Dar es Salaam kutonunua eneo wala kuendeleza ujenzi bila kuwasiliana na wataalamu wa ardhi wakati Mpango Kabambe utakapoanza kutekelezwa.
Naye Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Mhe. Isaya Mwita amewaomba viongozi wa Serikali za Mitaa pamoja na Madiwani wote wa Jiji la Dar es Salaam kutoa ushirikiano kwa wataalamu ili wananchi waweze kutoa maoni yao kuhusiana na mpango huo.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.